Wahudumu wa afya ya jamii katika Kaunti ya Kisii wamempongeza mwakilishi wa wanawake Sarah Otara kwa kuazisha kampeini ya kumaliza funza katika kaunti hiyo.
Wakiongea Jumatatu katika mtaa wa mwembe, wakiongozwa na mwenyekiti wao Kepha King’oina, walisema wako tayari kushirikiana na mwakilishi wa wanawake kwa kampeini hiyo ambayo ni ya kuwasaidia watu walioathirika na funza.
“Sisi kama wahudumu ya afya ya jamii tunampongeza mwakilishi wa wanawake kwa mradi huu. Tutashirikiana naye ili kuhakikisha kuwa funza wameisha katika kaunti yetu,” alisema King’oina.
Aidha, walisema kuwa wamekuwa wakiwaomba viongozi kujitokeza na kuwasaidia watu walioathirika katika jamii na sasa wanaimani kuwa viwango vya kuwasaidia vitaongezeka kwa kampeini hiyo ambayo imeazishwa na mwakilishi huyo.
“Sisi hupitia changamoto nyingi wakati tunapowatembelea waathiriwa lakini kutokana na mradi huu wa mwakilishi wa wananawake, natumai kuwa shida hizo zitaisha na waathiriwa watasaidika pakubwa,” aliongezea King’oina.
Kwingineko, waliwaomba watu wanaoathiriwa katika familia kujitokeza na kuripoti hali yao ili waweze kufikiwa na mradi huo wa kuwasaidia waathiriwa.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa kuna baadhi ya familia haswa huko mashinani ambazo hazitaki kukubali kuwa watu wao wameathiriwa na funza, jambo ambalo huwazuia kupata msaada mapema.
Kepha alisema kuwa watoto na wazee ndio wameathirika zaidi kutokana na hali duni ya maisha na kutojali kwa wazazi au walezi wao na kuwaomba wakazi wa eneo hilo kuwajibika katika familia ili kumaliza janga la funza.