Mwenyekiti wa muungano wa wakimbizi wa ndani kwa ndani katika eneo la Nyanza, Nelson Owegi, amependekeza kufanywa uteuzi mpya wa wawakilishi wa wakimbizi walioathiriwa na ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2007, hasaa katika Kaunti ya Migori.

Share news tips with us here at Hivisasa

Katika mahojiano na mwandishi huyu siku ya Alhamisi, Owegi alisema kuwa ameghadhabishwa na hali ya watu wasiokuwa wakimbizi kuteuliwa kuwa wawakilishi wa wakimbizi hao.

Kauli ya Owegi inajiri kufuatia kikao cha wawakilishi wa wakimbizi wa eneo la Nyanza kilichofanywa mnamo Aprili 9, katika Kaunti ya Migori, ambapo swala hilo liliangaziwa.

Owegi alisema kuwa kulingana na katiba, sheria hairuhusu watu ambao sio wakimbizi kuwa wawakilishi wa wakimbizi, kwa kuwa hawatambui changamoto zinazowakabili wakimbiza husika.

Owegi pia alitoa wito kwa serikali kuu kuwatendea haki wakimbizi wa ndani kwa ndani hasaa kufuatia ahadi waliopewa baada ya operesheni Rudi Nyumbani, iliyochangia wakimbizi wa ndani kwa ndani kuondoka katika kambi za wakimbizi na kurejea kwao.

“Serikali iliahidi kuhakikisha kuwa wakimbizi wote wa ndani kwa ndani nchini wanafidiwa ila zoezi hilo limeishia kufanywa kwa mapendeleo, na hivyo tungali tunasubiri kupewa fidia,” alisema Owegi.