Kamati ya hesabu za umma (PAC) inalitaka bunge la kitaifa kupunguza idadi ya makamishna wa IEBC hadi watatu.
PAC inataka bunge pia wabadili namana ya uteuzi katika tume hiyo na wagawanye majukumu yao na yale ya makatibu wakuu. Kamati hiyo imesema kuwa vigezo hivi vitatu vina umuhimu mkubwa haswaa katika kuupa uchaguzi mkuu ujao umuhimu unaohitajika na kuepuka mizozo kama iliyojiri kwenye chaguzi kuu mbili zilizopita.
Iwapo mabadiliko hayo ya kisheria yaliyopendekezwa na PAC yatatekelezwa basi uongozi wa tume ya IEBC utaathirika haswaa masuala ya kifedha na tume hiyo kujisimamia kibinafsi.
‘‘Hasa, uadilifu wa mchakato wa kupiga kura ni lazima uangaziwe kwa undani ili kuwezesha matokeo ya uchaguzi kuwa ya kweli na huru na ya haki kwa mwananchi,’’ ripoti hiyo ya PAC ilisema.
Ripoti hiyo iliyotolewa na PAC pia imedai kuwa mwenyekiti wa IEBC, Isaack Hassan aliathiri pakubwa shuguli za kila siku za tume hiyo na pia alihusika pakubwa na kufeli kwa mpango wa kununua mitambo ya BVR. Tume hiyo pia imeweka wazi kuwa makamishna wa IEBC walikuwa na wakati mgumu kuelezea kamati ya PAC kuhusu majukumu yao ya kila siku na jinsi wanavyoyaendeleza.
PAC imeagiza bunge la kitaifa kuangazia suala hili kwa haraka huku ikisisitiza kuwa ni lazima mfumo wa kuwateua makamishna wa IEBC uondolewe.
Tume hiyo imependekeza kuwa uteuzi wa kamishna lazima uhusishe wadau wote husika kwa kuzingatia umoja wa taifa.