Wakulima katika kaunti ya Nakuru wametakiwa kupanda vyakula mbadala vinavyositahimili ukame ili kujiepusha na makali ya njaa haswa wakati wa kiangazi.

Share news tips with us here at Hivisasa

Afisa mkuu katika wizara ya kilimo, Purity Wanja ametoa wito kwa wakulima kupanda vyakula vya jadi, alivyosema vinahitaji mvua ya kiwango cha chini ili kukomaa.

Akiongea wakati wa siku ya kilimo katika wadi ya Bahati siku ya Alhamisi, Wanja alisema kuwa kutegemea sana  kilimo cha mahindi ndicho chanzo cha uhaba wa chakula nchini, kwani mahindi hutegemea mvua ili kunawiri

“Tumetegemea sana mahindi kwa muda mrefu na hiyo imepelekea ukosefu wa chakula katika taifa. Kupanda mahindi kwa muda mrefu pia kumeharibu rotuba mashambani na hii imepelekea kupungua kwa mazao,” alihoji Wanja.

“Ni vyema turudie vyakula vya kiafrika kama mawele, wimbi, mihogo, viazi vitamu, njugu, parachichi, papai na mboga za kienyeji ili kukabili uhaba wa chakula,” alisema Wanja.

“Vyakula hivi nilivotaja havihitaji mvua nyingi ili kukua na hata vinaweza kunawiri wakati wa kiangazi,” aliongezea kusema.

Afisa huyo aidha alisema kuwa serikali ya kaunti iko tayari kutoa mbegu za vyakula hivyo kwa wakulima wanaotaka kuvipanda.

“Tunatoa mbegu za vyakula vya kienyeji na mbolea kwa wakulima ili waweze kuvipanda kando na kupanda mahindi waliozoea,” alisema.

Aliwataka wakulima kutumia vyema mahindi waliovuna kwa kuwa kiangazi kinachoshuhudiwa huenda kikafika hadi mwezi Aprili.