Viongozi wa mrengo wa Cord pamoja na gavana ambao wanaendeleza kampeini ya Pesa Mashinani lengo lao kubwa ni kulinda ugatuzi.
Seneta wa Kaunti ya Homa-Bay Moses Kajwang’ ambaye alihutubia wakaazi mjini Molo akiandamana na maseneta wa kamati ya seneti kuhusu barabara na uchukuzi amesema baadhi ya maeneo nchini yamebaki nyuma kimaendelea huku mgao ambao unaelekezwa kwa Serikali za gatuzi kutoka hazina ya kitaifa ukielemewa kufadhili kikamilifu maendeleo ya Serikali za majimbo.
Seneta Kajwang’ amesema kuwa kinyume na ilivyokuwa kabla ya uwepo wa Serikali za kaunti, wananchi kote nchini walilkuwa wanategemea Serikali Kuu kwa ukarabati wa barabara muhimu, uwepo wa huduma bora za afya pamoja na elimu.
Seneta huyo amesema Serikali za kaunti zina mzigo mkubwa wa kuendeleza shughuli zake huku asilimia kubwa ya bajeti zao ikitumika kwa kuwalipa wafanyikazi mishahara pamoja na shughuli za kusimamia kaunti hizo.
“Lengo la kuuliza pesa zaidi kutoka kwa Serikali Kuu ni kulinda ugatuzi na kuhakikisha kwamba Serikali za maeneo zinaweza kujisimamia na kugatua huduma za maendeleo haswa katika kaunti ambazo zimebaki nyumba kimaendeleo tangu Kenya ijinyakulie uhuru wake,” alisema Kajwang’ akiwa mjini Molo.
Aidha, alisema ni kwa sababu hizo ambazo wanaCord na magavana wanapigania uwepo wa hazina kubwa kuelekezwa mashinani ili kuwamalizia wananchi kero la matatizo yaliyoko katika kaunti zao.
Kiongozi huyo alitamatisha kwa kusema kuwa Bunge la kitaifa linaweza kushinikiza fedha zaidi kutengewa Serikali za kaunti, lakini akasema uwepo wa wabunge wachache ambao wanania hiyo kwenye bunge la kitaifa ndio kinachochea kampeini ya Pesa Mashinani.
Kajwang’ aliendeleza wazo hilo katika kituo ambapo wanachama wa kamati hiyo iliyokuwa ikizuru barabara ya Molo-Olenguruone ilipofanya vikao na wananchi.
Maeneo hayo ni pamoja na vituo vya kibiashara vya Kibunja, Molo mjini, Muchorwe, Seguton, Mwangati, Keringet, Amalo, Olenguruone na Kiptagich.