Rais Uhuru Kenyatta ameshinikizwa kwa pakubwa kuvunjilia mbali bodi ya kusimamia hazina ya vijana YEDF.
Hii ni kufuatia madai kuwa bodi hiyo ilifeli kuzuia kupotea kwa takriban sh180 milioni katika hazina hiyo ya vijana.
Kamati ya bunge kuhusu uwekezaji, (PIC) na tume ya ukaguzi wa mashirika ya umma zimependekeza kuondolewa kwa bodi hiyo ili kewezesha kufanyika kwa uchunguzi. Hata hivyo, miezi sita baada ya madai ya ufisadi kuibuka katika hazina ya vijana, bodi ya kusimamia hazina hiyo bado ipo ofisini licha ya kuwa mapendekezo ya kuondolewa kwa bodi hiyo yaliwasilishwa kwa Rais Uhuru Kenyatta ili kuiwezesha tume ya maadili na kupambana na ufisadi nchini EACC na mashirika mengine ya kupigana na ufisadi kuchunguza kupotea kwa fedha hizo.
Wiki iliyopita, waziri wa masuala ya vijana na jinsia, Sicily Kariuki aliifahamisha kamati ya PIC kuwa mapendekezo ya kuitaka bodi hiyo kuondolewa yaliwasilishwa kwa Rais Kenyatta ila bado hajafanya lolote kuhusu mapendekezo hayo.
‘‘Tumemrai Rais Kenyatta kupitia kwa mkuu wa utumishi wa umma kuwa bodi ya hazina ya vijana inafaa kuondolewa ili kuwacha nafasi kwa uchunguzi kuendelezwa,’’ Bi Kariuki alisema.
Bodi ya hazina ya vijana na uongozi wa hazina hiyo ukiongozwa na Bruce Odhiambo na aliyekuwa afisa mkuu mtendaji Bi Catherine Namuye, imedaiwa wakati wa uchunguzi na kamati ya PIC, inayoongozwa na mbunge wa Eldas, Adan Keynan kuwa ilifeli kuzuia kupotea kwa fedha hizo za umma ilhali walikuwa na uwezo wa kukinga ubadhirifu huo wa fedha ambazo zilikuwa zimetengwa kuwawezesha vijana nchini Kenya kuanzisha miradi ya biashara ili kujiendeleza kimaisha na kukabiliana na umaskini.