Wawakilishi wadi wa muungano wa Cord ambao ndio walio wengi katika bunge la kaunti ya Kisii wamemteua kiongozi wa wengi ambaye atashikilia wadhifa huo kwa mda hadi kesi iliyoko mahakamani ya kupinga kuondolewa mtangulizi wake kukamilika.
Mwakilishi wa wadi ya Kitutu Central Pius Abuki aliteuliwa kuchukua wadhifa huo baada ya wawakilishi wa muungano huo wa Cord kupendekeza mwakilishi huyo kuchukua wadhifa huo.
Aliyekuwa katika wadhifa huo hapo mbeleni Protus Moindi alielekea mahakamani kupinga kuondolewa kwake baada ya idadi kubwa ya Wawakilishi wa wadi katika bunge hilo kupoteza imani naye na kumwondoa.
Spika wa bunge la kaunti ya Kisii Okerosi Ondieki hii leo alitangaza Mwakilishi Pius Abuki kushikilia wadhifa huo hadi kesi iliyoko mahakamani itakapo amuliwa.
“Wanachama wa ODM ambao ndio wengi katika bunge hili wamemteua Pius Abuki kuwa kiongozi wa wengi lakini atakuwa kwa mda hadi kesi itakapoamuliwa," alisema Ondieki.
"Basi nitatangaza tena Pius Abuki kuwa kiongozi wa walio wengi kikamilifu,” aliongeza Ondieki.