Chama cha PNU (Party of National Unity) kinanuia kufanya mazungumzo na Balozi wa Kenya nchini Tanzania Chirau Ali Mwakere ili kujadili uwezekano wa kujiunga na chama hicho.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Haya ni kwa mujibu wa naibu mwenyekiti wa kitaifa wa chama hicho Sheikh Juma Ngao, aliyesema kuwa chama hicho kina mipango thabiti ya kujiwakilisha katika nyadhfa mbali mbali ifikapo uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.

Sheikh Ngao alisema kuwa wanatarajia kusimamisha wawaniaji wakakamavu kwa tiketi ya chama cha PNU mwaka wa 2017.

Akizungumza na wanahabari siku ya Jumapili katika hoteli moja jijini Mombasa, Ngao alisema kuwa licha ya duru zilizoenea kuwa Mwakwere ameasi chama cha Jubilee na kujiunga na ODM, hali hiyo haitawazuia kufanya mazungumzo ya kumvutia na kumuandikisha kama mwanachama wao.

“Chama sio kibla ambacho waumini wa Kiislamu wanaelekea wakati wanaposwali. Mtu anaweza badili wakati wowote anapohisi sera hazimfaidi,” alisema Ngao.

Aidha, Ngao alisema kuwa chama hicho kimejiandaa vilivyo kuona kuwa kinachukua hatamu ya uongozi nchini, na kuepua wananchi kutokana na siasa potofu za ubaguzi, upendeleo na ufisadi.

Akiyataja baadhi ya maendeleo yaliyotokana na chama hicho kuanzia kwa kupitishwa kwa katiba mpya na ugatuzi na miundo msingi nchini, Ngao alisema kuwa chama hicho ndicho chombo kitakachowakomboa Wapwani kutokana na dhulma na kuwahakikishia maendeleo wanayostahili.

Vile vile, alisema kuwa PNU itatoa nafasi za uwanachama kwa yeyote yule, ili kuhakikishia wananchi maendeleo na uwakilishi katika ngazi tofauti serikalini.

Aidha, alisema kuwa mipango imekamilika ya kufungua afisi za chama hicho katika Kaunti ya Mombasa, Kwale na Kilifi ili kusahilisha oparesheni za chama hicho katika Ukanda wa Pwani.