Polisi katika eneo la Subukia siku ya Jumapili walimtia mbaroni Polisi bandia mmoja akiwa na pingu pamoja na kitambulisho bandia cha shirika la ujasusi nchini almaarufu NIS.
Edward Mbugua Njihia aliye na umri wa miaka 37 alitiwa nguvuni katika kituo cha kibiashara cha Kabazi mwendo wa saa mbili jioni na Maafisa wa upelelezi.
Akithibitisha tukio hilo, Mkuu wa Polisi katika eneo la Subukia Alex Ng’ang’a alisema kuwa mshukiwa huyo alipatikana na kitambulisho bandia cha Afisa wa shirika la NIS pamoja na pingu wakati Maafisa hao wa Polisi walipoendeleza msako nyumbani mwake katika kitongoji duni cha Milimani.
“Wananchi walitupasha habari kuhusu jamaa huyo ambapo tulianza kumchunguza na kumpata na hatia hizo. Punde tu uchunguzi zaidi kumhusu utakapokamilika, mshukiwa atafikishwa Mahakamani mara moja,” alisema Ng’ang’a.
Wakaazi katika kituo hicho cha kibiashara wamedai kuwa jamaa huyo anafahamika vyema kuwa mhubiri wa Kanisa moja katika eneo hilo, huku kukiwa na ripoti kuwa tayari alikuwa ametawazwa kuwa Kasisi.
Tukio hilo liliwashangaza waumini wengi wa dhehebu hilo kwani hawakudhania kuwa Kasisi huyo alikuwa Polisi bandia, kwani alikuwa akiongoza ibada za Jumapili kila wiki.
“Ninazidi kuwahimiza wakaazi wa eneo hili kuwa macho na kuwapasha habari muhimu Polisi kuhusu wahalifu au wanapo shuku watu ambao hawana ufahamu kuwahusu ili hatua mwafaka ziweze kuchukuliwa haraka iwezekanavyo,” aliongeza Afisa Ng’ang’a.