Share news tips with us here at Hivisasa

Mkuu wa polisi katika kituo cha Keroka, Kaunti ya Nyamira Peterson Nyongeza amekanusha madai kuwa maafisa wa kituo hicho wanazembea kazini kwa kutowajibikia kazi yao kikamilifu.

Hii ni baada ya wakazi wa keroka kujaribu kuandamana siku ya Jumanne katika mji wa Keroka, wakilalamikia ukosefu wa usalama katika eneo hilo, baada ya mtu mmoja kuawa mita chache kutoka kwa kituo hicho cha polisi cha Keroka.

Akizungumza siku ya Jumanne na waandishi wa habari katika mji wa Keroka, mkuu huyo wa polisi alisema kuawa kwa mtu huyo ambaye ni mfanyi biashara katika mji huo ni visa vya kila mara.

Alisema kuwa kisa hicho hakikusababishwa na maafisa wa polisi kutowajibikia kazi yao kwani visa vya mauaji ya aina hiyo vimekuwa vikishuhudiwa kila wakati katika eneo hilo.

“Inasemekana kuwa mtu huyu ambaye aliuwawa alikuwa na shilingi 70,000 ambazo zilichangishwa ili kugharamia mazishi ya mwenzao. Huenda pesa hizo ndizo zilimsababishia kuuliwa,”alisema Nyongeza. 

Wakazi na wafanyi biashara wa mji wa Keroka waliamua kuunda kamati ya watu 13 ambao watakuwa wakiangalia masuala ya usalama kwani wanadai maafisa wa polisi hawajawasaidia kamwe.

“Kwa miezi mitatu iliyopita watu 30 wameuwawa katika eneo hili la keroka. Tutaendelea kuhesabu watu wangapi kwa mwaka?Tumeamua kuunda kamati yetu ili iwe inaangalia masuala ya usalama katika eneo hili,” alisema Cliff Ong’era, mkazi.