Maafisa wa polisi wa eneo la Kikuyu wanaendeleza msako mkali dhidi ya kundi la majambazi waliomuua mfanyibiashara mmoja nyumbani kwake.

Share news tips with us here at Hivisasa

Inadaiwa kuwa majambazi hao walimpora mfanyibiashara huyo mali ya thamani isiyojulikana katika eneo la Ondiri, Kikuyu.

Akidhibitisha kisa hicho siku ya Alhamisi, mkuu wa polisi katika eneo la Kikuyu Mutune Maweu alisema kwamba mfanyibiashara huyo alivamiwa kwake na majambazi waliokuwa wamejihami na bunduki na panga.

Alisema kwamba majambazi hao watano walimpiga mlinzi wa nyumba ya marehemu na kumfunga kwa kamba kabla ya kuingia hadi chumba cha kulala cha marehemu.

Maweu alielezea kwamba washukiwa waliitisha pesa na walipopewa, walipora mali za thamani kabla ya kumuua mfanyibiashara huyo na pia kumdhulumu kimapenzi mkewe kabla ya kutoroka.

Alieleza kwamba polisi walifika pale muda mfupi baada ya kisa hicho na kumpeleka mke na mlizi wa marehemu hospitalini nao mwili wa marehemu ukapelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Kikuyu.

"Uchunguzi umeanza kufuatia kisa hicho na polisi watafanya kila juhudu kuhakikisha kwamba washukiwa wamekamatwa. Walioshuhudia kisa hicho akiwemo mlinzi wa nyumba ya marehemu wameandikisha taarifa kituoni na uchunguzi unaendelea," alisema Maweu.