Idara ya usalama imetakiwa kuwachunguza wafanyibiashara wanaojihusisha na uuzaji wa kanda za video nyakati za usiku katika eneo bunge la Kisauni.
Hatua hii inajiri baada ya visa vya watoto kuripotiwa kupatikana wakiwa wamebakwa ndani ya vibanda vya wafanyibiashara hao, hasa katika eneo la Mshomoroni.
Akizungumza na mwanahabari huyu siku ya Jumatano, Salim Juma, mkaazi wa Makumba, alisema kuwa visa hivyo vimeongezeka katika sehemu hiyo, kisa cha hivi majuzi kikiwa kubakwa kwa mototo wa miaka sita ndani ya kibanda kimoja katika eneo hilo.
Aidha, alitaja kupotea kwa umeme kila mara kama chanzo kikuu cha kuongezeka kwa visa sawia na hivyo katika eneo hilo.
Vilevile, Juma aliwashauri wazazi kuwahusisha viongozi wa mashinani katika masuala ya ubakaji ili wapate usaidizi unaofaa.
Aidha, amewataka wazazi kutoa ripoti kwa maafisa wa polisi kuhusu washukiwa wa ubakaji, ili kurahisha kukamatwa kwao.