Afisa wa polisi amefikishwa kizimbani kwa kosa la kumpiga na kumjeruhi kijana mmoja pasi na sababu mwafaka.
Afisa huyo, Timo Onyanyi, anadaiwa kushambulia Abdalla Swale kwa magumi na kumjeruhi kichwani na mkononi, katika eneo la Matuga, Kaunti ya Kwale, mnamo Julai 18, mwaka huu.
Mshukiwa huyo alikanusha mashtaka hayo mbele ya Hakimu Viola Yator katika Mahakama ya Mombasa siku ya Alhamisi.
“Sikuhusika kabisa katika kumshambulia kijana huyo,” alisema Onyanyi.
Mahakama imemuachilia afisa huyo kwa dhamana ya shilingi elfu hamsini.
Kesi hiyo itasikizwa mnamo Agosti 9, 2016.