Maafisa wa polisi mjini Mombasa wanachunguza uhusiano kati ya Gavana Hassan Joho na mshukiwa mkuu wa ulanguzi wa dawa za kulevya Ibrahim Khatri.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mshirikshi mkuu wa ukanda wa Pwani Nelson Marwa alisema kuwa maafisa hao wanalenga kubaini sababu zilizomsukuma Joho kuenda katika kituo cha polisi cha Urban na kuamrisha polisi kumwachilia huru mshukiwa huyo.

Khatri anadaiwa kuhusika katika ulanguzi wa mihadarati pamoja na wizi wa magari nchini Uingereza.

Marwa alimkosoa Joho kwa kuhitilafiana na uchunguzi unaoendelezwa na maafisa wa polisi, na kuongeza kuwa gavana huyo pia atafanyiwa uchunguzi.

Kulingana na ripoti ya polisi, Khatri alinaswa na bunduki tatu nyumbani kwake katika eneo la Ganjoni, alipotiwa mbaroni siku ya Ijumaa, juma lililopita.

Maafisa wa usalama katika makao makuu ya polisi huko Kizingo wamekana kumtia nguvuni Joho, licha ya gavana huyo kusisitiza kwamba alitiwa mbaroni na kuzuiliwa pasipo sababu zozote za msingi kabla ya kuachiliwa huru.