Idara ya usalama imesema kuwa inapania kuwaongeza maafisa wa polisi wanaoshika doria nyakati za usiku katika eneo la Kisauni, Kaunti ya Mombasa.

Share news tips with us here at Hivisasa

Maafisa hao wanatarajiwa kusaidiana na wenzao ambao wanaendesha oparesheni ya kukabiliana na wizi wa mabavu unaotekelezwa na makundi ya vijana eneo hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Ijumaa Kamanda wa polisi eneo la Pwani Francis Wanjohi alisema kuwa hatua hiyo ni njia moja wapo ya kuhakikisha kuwa visa vya utovu wa usalama katika Kaunti ya Mombasa vinakabiliwa vilivyo ili kuwapa wenyeji mazingira bora.

Akitoa mfano wa hivi majuzi ambapo vijana wawili waliohusishwa na uhalifu waliuawa na polisi, Wanjohi alisema kuwa maafisa wake wataendelea kuimarisha usalama eneo hilo ili kuzuia hali ya taharuki haswa wakati huu wa Ramadhan.

Kamanda huyo aliwasihi wenyeji kushirikiana kwa kutoa taarifa kuhusu washukiwa wa uhalifu kwa maafisa wa usalama.

Aidha, aliwaonya vijana wanaojihusisha na visa hivyo akisema kuwa watakabiliwa na mkono wa sheria.