Idara ya polisi nchini imetangaza kuwa itatoa shilingi milioni mbili kwa yeyote atakaye toa taarifa muhimu kuhusiana na waliko jamaa wawili wanaodaiwa kupanga shambulizi la kigaidi humu nchini.
Akizungumza siku ya Jumatano, Inspekta Mkuu wa Polisi Joseph Boinnet alisema kuwa jamaa hoa wanaofahamika kama Ahmed Hish na Farah Dagane, ambao wanasomea udaktari, walifanikiwa kutoroka katika Hospitali ya Kitale baada ya kugundua kuwa walikuwa wanasakwa na maafisa wa polisi.
Aidha, Boinnet alisema kuwa polisi walifanikiwa kumkamata mwenzao anayefahamika kama Mohammed Ali, ambaye pia anajifunza kuwa daktari katika Hospitali ya Wote, Kaunti ya Makueni.
Kwa mujibu wa Boinnet, jamaa huyo alifikishwa mahakamani siku ya Jumanne na atazuiliwa kwa siku 30 ili kutoa nafasi kwa maafisa wa polisi kuendeleza uchunguzi zaidi dhidi yake.