Polisi mjini Mombasa wameanza msako dhidi ya wanaohusika katika biashara ya ukahaba.
Haya yanajiri baada ya wakaazi katika eneo la Likoni kulalamikia ongezeko la biashara hiyo katika eneo hilo.
Akizungumza siku ya Alhamisi, mkuu wa polisi eneo la Likoni Bwana Willy Simba alisema kuwa wakaazi wa eneo hilo kwa muda sasa wamekuwa wakilalamikia ongezeko la makahaba.
Simba alisema kuwa hali hiyo inasikitisha kwa kuwa baadhi ya makahaba hao ni wasichana wadogo wenye umri wa kwenda shule.
Akizungumza katika Kituo cha Polisi cha Likoni, Simba alisema kuwa maafisa wa polisi hawataruhusu tabia hiyo kuendelea katika eneo hilo.
Afisa huyo aliahidi kuanzisha oparesheni ya kuwakamata wasichana hao kama njia moja ya kukomesha biashara hiyo.
"Kama wazazi, tunapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuwaonya watoto dhidi ya kujihusisha na biashara hii. Maafisa wangu watahakikisha kwamba hakuna ukahaba utakao endelea hapa Likoni,” alisema Simba.
Simba alisema kuwa hali hiyo imechangiwa na wazazi wanaokosa kuwajibikia majukumu yao kama inavyostahili.
"Wazazi Likoni wanapaswa kuchukua udhibiti kamili wa familia zao na kuwaonya wanao dhidhi ya biashara ya ukahaba,” alisema Simba.