Idara ya usalama mjini Mombasa imewaonya vijana wanaowahangaisha wazee wa mitaa hasa katika eneo la Likoni.
Polisi wamesema kuwa watakaopatikana na hatia watakabiliwa kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Mkuu wa polisi katika eno la Likoni Willy Simba alisema kuwa tayari wamepata ripoti kuhusiana na njama za vijana hao, na kuwa watachukuliwa hatua kali za kisheria.
“Tayari tumepata ripoti kuwa kuna makundi ya vijana yanoyowahangaisha wazee wa mtaa. Nataka niwaambie kuwa ukipatikana utajilaumu mwenyewe,” alisema Simba.
Kauli ya afisa huyo wa usalama inajiri baada ya wazee wa mitaa mbalimbali katika eneo la Likoni kulalamikia kuvamiwa na vijana wanaodai kuwa wamewasaliti kwa kutoa ripoti za kuwahusu kwa idara ya usalama.
Wengi wa vijana hao wanadaiwa kuwa miongoni mwa vijana wanaowahangaisha wenyeji wakitumia mapanga, visu na vifaa vingine butu.