Maafisa wa polisi katika eneo la Likoni, Kaunti ya Mombasa, wanaendeleza oparesheni dhidi ya kundi la kihalifu linalofahamika kama ‘Kapenguria six’.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Afisa mkuu wa polisi eneo la Likoni Willy Simba, amesema kwamba tayari washukiwa wanne wa kundi hilo wamefikishwa mahakamani baada ya kutiwa nguvuni.

Wanne hao wameshtakiwa kwa kosa la wizi wa mabavu katika ufukwe wa Bahari Hindi wa Shelly.

Akizungumza katika kituo cha Polisi cha Likoni siku ya Jumatatu, Simba alisema kwamba pia watakabiliana na makundi mengineyo ya kihalifu yanayowahangaisha wakaazi katika Kaunti ndogo ya Likoni.

"Tunaendelea kuwasaka wahalifu wanaowahangaisha wakaazi wa Likoni ili kuimarisha usalama katika eneo hili. Tunawaomba wakaazi kushirikiana na polisi kwa kutoa habari kuhusu washukiwa ndio wakabiliwe barabara,” alisema Simba.

Simba alisema kwamba maafisa wa polisi wanaendeleza upelelezi kuhusiana na kuchipuka kwa makundi ya kihalifu katika eneo zima la Likoni, kwa lengo la kuhakikisha kwamba Kaunti hiyo ndogo ni salama kabla ya siasa na kampeni za mwaka wa 2017 kupamba moto.