Naibu Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Salim Mahmoud amewataka maafisa wa polisi mjini humo kukoma kuwahangaisha waraibu wa mihadarati ambao tayari wameasi matumizi ya dawa hizo na kuanza kurekebisha tabia.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Akizungumza katika hafla iliyowaleta pamoja waathiriwa wa dawa za kulevya kutoka sehemu mbalimbali katika ukanda wa Pwani siku ya Jumanne, Mahmoud alisema kuwa serikali itawapa vibali vijana ambao tayari wamejiunga na vituo vya kurekebisha tabia ili maafisa wa usalama waweze kuwatambua kwa urahisi.

“Ni vigumu kwa maafisa wetu kubaini kati ya wanaotumia dawa na walioasi matumizi wa dawa hizi. Kwa hivyo tutatoa hamasa kwa maafisa wetu na pia tutoe vibali kwa vijana wanaotumia dawa za kujirekebisha tabia,” alisema Mahmoud.

Aidha, Mahmoud alisema kuwa serikali itawapa ajira waathiriwa ambao tayari wameirejelea hali yao ya kawaida ili kuwasaidia kujikimu kimaisha, na kupunguza uwezekano wao kurejelea utumizi wa dawa hizo.

Kwa upande wao, vijana hao waliitaka serikali kujenga vituo vya afya katika miji mbali mbali katika ukanda wa Pwani, ili kuwawezesha kupata huduma wa haraka.