Maafisa wa polisi mjini Mombasa wamewatia nguvuni vijana 17 wanaodaiwa kujihusisha na uhalifu na kuwahangaisha wakaazi wa Mombasa.
Kulingana na Naibu Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Mahmuod Salim, wengi wa vijana hao ni wa kati ya umri wa miaka 12 hadi 26.
Salim alisema kuwa wengi wao wamejiunga na makundi ya kihalifu kutokana na uraibu wa utumizi wa mihadarati.
Akizungumza afisini mwake mjini Mombasa siku ya Jumapili, Salim alisema kuwa vijana hao walitiwa nguvuni usiku wa kuamkia siku ya Jumapili kwani wengi wao hukita kambi katika vituo vya kuabiri magari ya uchukuzi wa umma na kuvamia wananchi.
Alisema kuwa serikali iko macho kuhakikisha kuwa usalama wa mwananchi unadumishwa vyema na makundi yanayochipuka ya kihalifu yanakabiliwa barabara na maafisa wa polisi.
"Tuliwanasa vijana hao katika maeneo ya Buxton wakiwa wamejihami kwa silaha ikiwemo panga na vifaa vingine hatari. Tunawazuilia kisha tutawafikisha mahakamani,” alisema Salim.
Afisa huyo aliwataka wakaazi kuhakikisha kuwa wanatoa habari kuhusu washukiwa wa uhalifu kwa maafisa wa polisi ili watiwe nguvuni.