Polisi Nyamira wameanzisha uchunguzi dhidi ya washukiwa wawili waliotoweka nakuliacha gari lao lililokuwa na mihadarati katika barabara kuu ya Kisii-Nyamira, eneo la Sironga.
Akithibitisha kisa hicho siku ya Jumatano, afisa msimamizi wa doria kwenye Kaunti ya Nyamira Ken Kiptanui alisema kuwa washukiwa hao walitoweka kwa miguu walipogundua kuwa polisi walikuwa wakiwafuata.
Kiptanui alisema kuwa mihadarati hiyo iliyokuwa imefungwa kwenye gunia ilikuwa ikisafirishwa kwenda eneo lisilojulikana.
Alisema kuwa uchunguzi umeanzishwa kubaini washukiwa hao walivyo fanikiwa kupita kwenye vizuizi vingine vya polisi bila kugundulika.
"Tungali tunawasaka washukiwa wa mihadarati hii kwa kuwa walitoweka kwa miguu baada yao kugundua kuwa maafisa wa polisi walikuwa wakiwaandama. Tunalotaka kufahamu ni vipi washukiwa hawa walivyopita kwenye vizuizi vya polisi. Huenda mihadarati ambayo tumeinasa ilikuwa ikisafirishwa kutoka nchini Tanzania kwenda jijini Nairobi,” alisema Kiptanui.
Afisa huyo aidha amesihi umma kuwasilisha ripoti kwa hiari kwa maafisa wa polisi kuhusiana na waliko washukiwa hao akiongeza kuwa watakaopeana arifa hiyo watalindwa.
Kiptanui aliwahimiza wakazi kushirikiana na polisi ili kuangamiza mihadarati ambayo inaendelea kuharibu maisha ya vijana.
"Wananchi wanastahili kuwa tayari kupeana ripoti kwetu kuhusiana na watu wanaoendesha biashara hii. Vilevile nawahimiza wananchi kushirikiana na vyombo vy usalama ili tuweze kuangamiza utumizi wa mihadarati miongoni mwa vijana wetu,” alisema Kiptanui.