Kamanda mkuu wa polisi ukanda wa Pwani Philip Tuimur katika hafla ya awali. Picha/ the-star.co.ke
Kamanda mkuu wa polisi ukanda wa Pwani Philip Tuimur amesema kuwa vita dhidi ya mihadarati vitaimarishwa hasa katika maeneo ya mipakani, viwanja vya ndege na katika Bandari ya Mombasa.Akizungumza katika kikao na wanahabari mjini Mombasa, Tuimur alisema kwamba imebainika wazi kuwa walanguzi wa dawa za kulevya wanatumia sehemu hizo kuendeleza biashara yao haramu.Alisema kuwa hawataruhusu biashara hiyo kuendelea, na kuongeza kuwa wataweka mikakati kabambe ya kukabiliana na walanguzi.Tuimur aidha aliongeza kuwa idara ya usalama ukanda wa Pwani inaendelea kufanya uchunguzi katika majumba ya wageni al maarufu villas, kwa kuwa idadi kubwa ya watalii wanatumia majumba hayo kuendeleza biashara hiyo haramu.“Kama idara ya usalama hatutalegeza kamba katika vita dhidi ya mihadarati hasaa katika ukanda wa Pwani, unaozidi kuathirika na janga hili,” alisema Tuimur.Haya yanajiri baada washukiwa 12 wa ulanguzi wa dawa za kulevya wakiwemo raia 4 wa kigeni kutiwa mbaroni siku ya Alhamisi katika maeneo tofauti ya ukanda wa Pwani.