Polisi wa trafiki katika barabara kuu ya Nakuru kuelekea Nairobi wanajibidiisha kuhakikisha hakuna ajali itakayotokea au maisha kupotea.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Hii ni kutokana na hatua ya abiria kupuuza maswala muhimu mojawapo ikiwa ni kufunga mshipi wakati wa usafiri.

Afisa mmoja wa kike wa idara ya trafiki kwenye barabara hiyo ambaye hakutaka kutajwa jina amesema, mshipi husaidia abiria kwa kuwadhabiti kwenye kiti endapo ajali itatokea au iwapo gari litakosa mwelekeo. 

Afisa huyo amedai kwamba kufunga mshipi huzuia asilimia kubwa ya majeraha mabaya ambayo yangetokea kama abiria hangejifunga mshipi.

Huku akitabasamu, amedhihirisha wito wa utumishi kwa wote akiwasaidia baadhi ya abiria kufunga mishipi yao iliyokuwa imekwama, jambo ambalo limewavutia abiria hao waliokuwa na wasiwasi kwani walihofia kukamatwa.

Hata hivyo, ametoa wito kwa wamiliki wa magari ya usafiri wa umma na yale ya kibinafsi kuhakikisha mishipi hiyo iko katika hali shwari na safi.

Hapo awali, barabara hii imekuwa kwenye vyombo vya habari kwa kusababisha ajali nyingi nchini haswa msimu wa krisimasi na sherehe nyinginezo.