Idara ya usalama katika eneo la Kisauni imeimarisha oparesheni zake za kiusalama katika eneo hilo kama juhudi za kusitisha makundi ya kihalifu ambayo yamekuwa yakiwahangaisha wakazi.
Afisa mkuu wa Polisi Kaunti ndogo ya Kisauni Richard Ngatia amesema kuwa oparesheni za kiusalama zinayalenga maeneo yaliyoorodhesha visa vingi vya uhalifu ili kuona kuwa wale wanaopanga na kutekeleza uhalifu wanatiwa nguvuni.
Ngatia ameyapuuza madai ya wakazi kuwa oparesheni hizo zimewalenga hata wale wasiokuwa na makosa, na akasisitiza kuwa maafisa wa usalama wanayazurui maeneo yaliyokiripoti ongezeko la visa vya kihalifu ikiwemo Bamburi, Mtopanga, Mwandoni na Mishomoroni.
Ngatia amewahimiza wakazi katika eneo hilo kutowaficha wahalifu miongoni mwao ili wakabiliwe kisheria na akadokeza kuwa makundi ya kihalifu yanayochipuka ni ya vijana wadogo wa miaka 14.
“Maafisa wa polisi wanaangazia maeneo yanatoka wahalifu lakini hawana nia yoyote na wakazi, hivyo basi sisi tutahakikisha tumekabiliana na wahalifu kikamilifu na kuimarisha usalama wa Kisauni na Mombasa kwa jumla,” alisema Ngatia siku ya Jumamosi.
Wakati huo huo, Afisa huyo wa Polisi amewataka wazazi kuwajibikia majukumu yao na kuhakikisha kuwa watoto wao wanapata elimu, huku akiwataka vijana katika eneo hilo la Kisauni kujitenga na uhalifu.