Polisi Changamwe wameanzisha msako dhidi ya magenge sugu yanaoendeleza visa vya uhalifu katika eneo hilo.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Hatua hii inajiri baada ya kikosi cha Flying Squad kuwapiga risasi washukiwa wawili wa ujambazi eneo la Miritini siku ya Jumapili.

Akizungumza siku ya Jumatatu, kamanda wa polisi eneo la Changamwe Stephen Cheteka, alisema kuwa vijana waliouawa walikuwa wahalifu sugu ambao wamekuwa wakiendeleza visa vya wizi wa mabavu.

"Hawa vijana ni wahalifu sugu na tutahakikisha tunawamaliza wote,” alisema Cheteka.

Cheteka alisema kuwa vijana hao wanaaminika kutekeleza kisa cha hivi majuzi ambapo walivamia mhudumu wa M-Pesa na kumuua mumewe.

Oparesheni hii inajiri baada ya kamishna wa Kaunti ya Mombasa Maalim Mohamed kuwataka wahalifu wote kujisalimisha kwa polisi.

Maalim aliapa kuwa maafisa wake watasambaratisha makundi yote ya wahalifu Mombasa.