Maafisa wa trafiki mjini Mombasa wameanzisha msako dhidi ya tuktuk zinazohudumu bila ya leseni na vibali vingine.
Akizungumza afisini mwake siku ya Alhamisi, kamanda wa trafiki katika kituo cha polisi cha Central mjini Mombasa Shem Aloo, alitoa amri kwa maafisa wake kushiriki msako huo.
Alisema kuwa wahudumu wa tuktuk wamekuwa na desturi ya kupuzilia mbali umuhimu wa kumiliki vibali hivyo.
Akitoa mfano wa tuktuk zilizonaswa siku ya Jumatano, Aloo alisema kwamba zaidi ya nusu ya tuktuk hizo zilikuwa hazina vibali kama vile leseni ya kuendesha biashara katikati mwa jiji la Mombasa.
Aidha, alisema kuwa idadi kubwa ya wahudumu hao hawakuwa na stakabadhi za kuonyesha kuwa wamehitimu kuendesha tuktuk hizo.
“Wengi wa wahudumu hao hujifunza kuendesha tuktuk hizo kwenye vichochoro, jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa abiria, kwani huwa wanakosa ufahamu wa sheria za trafiki,” alisema Aloo.
Kamanda huyo alisema kuwa wengi wao hawajajua hata maana ya taa zilizowekwa kwenye barabara, hali ambayo imekuwa ikisababisha msongamano wa magari na hata ajali.