Mbunge wa Msambweni Suleiman Dori katika hafla ya awali.[Photo/ the-star.co.ke]
Idara ya usalama Kaunti ya Kwale imeanzisha uchunguzi dhidi ya Mbunge wa Msambweni Suleimani Dori anayedaiwa kutoa matamshi ya uchochezi.Hii ni baada ya Dori kusema kuwa sharti eneo la Pwani lijitenge kutoka taifa la Kenya na kuanza kujisimamia kivyake.Aidha, Dori anadaiwa kuchochea wakaazi wa Kwale dhidi ya maafisa wa polisi.Mkuu wa polisi eneo la Msambweni Joseph Chebusit amesema hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya Dori ili awe mfano kwa viongozi wa kisiasa wanaoendeleza uchochezi katika jamii.Chebusit amesema uchunguzi wa kina umeanza dhidi ya matamshi hayo na hatua kali zitachukuliwa iwapo atapatikana na hatia.“Tunamchunguza na tutamkabili kisheria ili iwe funzo kwa wengine,” alisema Chebusit.Matamshi ya Dori yalijiri baada ya maafisa wa polisi kudaiwa kuwapiga wakaazi wa Ukunda na Mwabungo siku tatu zilizopita wakati wa oparesheni ya kutafuta bunduki zilizoibiwa katika shambulizi la kanisa la ACK Ukunda mwezi uliopita.Dori aliripotiwa kuongoza wakaazi kufanya maandamano baada ya operesheni hiyo ambapo kulingana na Chebusit, waandamanaji hao walivuruga na kuiba mali ya wafanyabiashara.