Maafisa wa polisi wamehimizwa kufanya uchunguzi na kuwatia mbaroni waliochochea ghasia zilizozuka katika mji wa Keroka siku ya Jumanne na kupelekea wengi kujeruhiwa.
Hii ni baada ya wakaazi kuzozonia mpaka kati ya kaunti ya Kisii na Nyamira na kupelekea wengi kujeruhiwa vibaya.
Wakizungumza siku ya Jumatano mjini Keroka Wawakilishi wa wadi katika kaunti ya Nyamira wakiongozwa na kiongozi wa walio wengi katika bunge la kaunti ya Nyamira Laban Masira na Beautah Omanga waliomba maafisa wa polisi kufanya uchunguzi na kuwatia mbaroni wachochezi wa ghasia hizo ili iwe funzo kwa wengine wanaopania kujihusisha na ulahgai huo.
“Kuna baadhi ya watu ambao walichochea ghasia mjini Keroka ambao walikuja na silaha kama mishale na panga, tunataka polisi wawachunguze na watiwe mbaroni,” alisema Masira.
Ghasia ambazo zilizuka mjini Keroka zimekuwa zikifanyika kufuatia mzozo wa mpaka ambapo maafisa wa kukusanya ushuru wa kaunti ya Kisii na wale wa Nyamira wamekuwa wakitofautiana ni wapi wanastahili kukusanyia ushuru katika soko la Keroka.
Kwa muda mrefu sasa magavana wa kaunti hizo mbili James Ongwae wa Kisii na John Nyagarama wa Nyamira wanahimizwa kutafuta suluhu lakudumu.