Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Polisi wa kituo cha Bahati wamelaumiwa pakubwa na wahudumu wa boda boda pamoja na vijana wanaofanya kazi kwenye timbo zilizo kwenye wadi za Bahati, Kiamaina na Kabatini, kwa kuwahangaisha pasi na sababu.

Wakizungumza na mwandishi huyu Jumamosi, wahudumu hao haswa wa kituo cha kibiashara cha Maili Kumi na Ahero, walisema kwamba vijana kadhaa wamevunjika viungo vya mwili kama miguu, baada ya kuanguka kwenye mashimo ya karakana hizo wakitorokea polisi.

Wito huo ulitiliwa mkazo na mwenyekiti wa wanabiashara eneo la Ahero Rafael Mwangi, aliyesema: “Vijana hawa wa kubeba mawe hutoroka wanapoona gari la polisi hata kabla ya lisimame, kwa sababu ya jinsi wamehangaishwa mbeleni. Wanapokamatwa wao hutakiwa watoe pesa ili kuachiliwa baada ya kusingiziwa kuwa wahalifu.”

Mhudumu wa bodaboda John Kamau alisema biashara yao inakuwa ngumu kufanya kutokana na kuhangaishwa na polisi, haswa ikiwa hawana leseni ama bima za pikipiki zao.

“Pikipiki hizi nyingi zimenunuliwa kwa mikopo ya benki. Kupata leseni, uwe na bima, kofia ya usalama, jaketi na kulipa ushuru kwa kaunti, imekuwa bei ghali kwa baadhi yetu. Hivyo polisi wa Bahati akikupata una kosa moja unapelekwa kwenye kituo cha polisi, na utaachiliwa ukitoa hongo,” alisema John aliyechangamoto polisi kuwafikisha mahakamani kama wana hatia.

Vijana hao wamemtaka naibu kaunti kamishna katika kaunti ndogo ya Bahati Kithinji Ithai, DO Macharia Njinu, na OCPD Duncan Nguthu kuwalazimisha polisi kufuata mkondo wa sheria katika kutekeleza majukumu yao.

Bwana Ithai tayari ameelekeza polisi kuacha kudhulumu wakaazi hao, akisema atakayeripotiwa kwake atachukuliwa hatua kisheria.