Mwanaharakati wa Nakuru Wycliffe Oguda, amelaumu polisi mjini Nakuru akisema wanajikokota katika kutekeleza haki kwa waadhiriwa mjini Nakuru .

Share news tips with us here at Hivisasa

Vile vile alisema kwamba kuna haja ya walinzi wanaopewa magavana na manaibu wao kufanyiwa usaili, ili kuhakikisha kwamba wanazingatia maadili wakiwa kazini na wanapotangamana na wananchi.

Oguda Ijumaa alikemea kisa ambapo askari mmoja mlinzi wa naibu gavana wa Nyamira Amos Nyaribo alimpiga risasi kidole mlinzi wa mkahawa hapa Nakuru baada ya askari huyo kuzozana na kidosho mnamo Jumatano.

Oguda alisema huo ni ukiukaji mkubwa wa haki za kibinadamu, na utumizi mbaya wa silaha.

“Huyu askari ambaye hajulikani kwa jina alikamatwa na wanaboda boda. Tungetaka kujua alizuiliwa katika kituo kipi cha polisi, na kama alipelekwa mahakamani kujibu mashtaka ya kuumiza na kuhangaisha raia,” Oguda alisema.

Oguda alisema hulka ya askari huyo mlinzi wa naibu gavana, inadhihirisha haja ya walinzi wa magavana na manaibu wao kuchunguzwa, na kubaini idadi inayofaa wapewe.

Kamanda wa polisi katika kaunti ya Nakuru Hassan Barua alidhibitisha kisa hicho kilichotokea siku mbili zilizopita katika hoteli ya Sideways barabara ya Kanu Street.

“Tumeanzisha uchunguzi ili kufahamu kilichosababisha David Ekoli Eworet ambaye ni mlinzi wa usiku apigwe risasi,” Barua alisema.