Maafisa wa polisi waliopatikana na makosa ya mauaji ya mtoto wa miaka 14, Kwekwe Mandaza, na kufungwa miaka saba gerezani wamekata rufaa kupinga kifungo hicho.

Share news tips with us here at Hivisasa

Veronica Gitai na Issa Mzee walipatikana na makosa ya mauaji hayo na kuhukumiwa kifungo cha miaka saba gerezani mnamo Februari 16, 2016 katika Mahakama kuu ya Mombasa.

Maafisa hao waliwasilisha rufaa hiyo kupitia kwa wakili wao Gerald Magolo siku ya Jumatatu, mbele ya jopo la majaji watatu; Jaji Mahandia Asike, Jaji Ouko William na Chatherana M’noti katika Mahakama ya rufaa ya Mombasa.

Majaji hao wameamua kuwa rufaa hiyo itasikizwa tarehe Mei 5, mwaka huu.

Itakumbukwa kuwa mnamo Februari 16 mwaka huu, Jaji wa mahakama kuu ya Mombasa Martin Muya aliwahukumu maafisa hao wa polisi kifungo cha miaka saba kila mmoja, baada ya kupatikana na hatia ya kumuua Kwekwe Mwendaza mnamo mwezi Agosti 2014, katika eneo la Kinango, Kaunti ya Kwale.