Aliyekuwa mwenyekiti wa chama cha TNA tawi la mji wa Nakuru daktari Abdul Noor, amekashifu polisi katika kaunti hiyo haswa wanaofanya doria za usiku mjini, kwa kuhangaisha wasafiri wanaoenda nyumbani wakati wa sherehe za Pasaka.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Akizungumza na mwandishi huyu mnamo Ijumaa, Noor alisema polisi mjini Nakuru wanaanzisha misako mwendo wa saa mbili kwa madai ya kudhibiti usalama, lakini wanaishia kuhangaisha wenyeji wa mji huo.

“Nimewasiliana na OCPD wa Central bwana Musa Kongoli, na kumfahamisha tabia ambayo polisi wake wameanzisha wakati huu wa pasaka. Watu wanakamatwa hata wakienda dukani saa mbili, na kuzungushwa mjini Nakuru kabla ya kufikishwa kituoni cha polisi saa nne,” akasema Noor.

Hata hivyo kulingana na Noor, rekodi ya watu wanaokamatwa kwenye misako aliyoita “haramu” haiwekwi kwenye kitabu cha matokeo (OB) ili wafikishwe mahakamani kulingana na sheria ila majina yao yanaandikwa kwenye kijikaratasi.

“Huu ni ukiukaji wa hali ya juu wa haki za kibinadamu, kwa sababu hakuna aliyefikishwa mahakamani. Wote wanaadikwa majina kwa karatasi sio kwa OB wakitoa hongo wanaachiliwa” akasema Noor.

Noor alisema mnamo Alhamisi jioni, baadhi ya maafisa waliokuwa wameandamana na gavana Kinuthia Mbugua katika ziara ya gavana mtaani mjini Subukia, walikamatwa saa moja unusu jioni walipokuwa wanatafuta mbinu za kuelekea nyumbani kati kati ya mji.

“Hata wafanyikazi wa gavana hawako salama, ilibidi tumpigie simu bwana Kongoli ili waachiliwe” akasisitiza dkt Noor.

Bwana Kongoli hakupatikana kujibu madai hayo kwani simu ya mwandishi huyu kwake haikujibiwa.