Wizara ya usalama imewaonya maafisa wa usalama dhidi ya mauaji ya kiholela.
Katibu mkuu katika Wizara ya usalama wa ndani Dkt Karanja Kibicho amesema hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya maafisa wanaojihusisha na mauaji ya kiholela nchini.
“Tutawachukulia hatua za kisheria polisi wanaotekeleza mauaji ya kiholela,” alisema Kibicho.
Akizungumza mjini Mombasa Kibicho alisisitiza kuwa lazima haki za binadamu ziheshimiwe maswala ya usalama yanapotekelezwa nchini.
“Kila Mkenya ana haki kikatiba na lazima haki hizo zilindwe,” alisema Kibicho.
Katibu huyo aidha alisema kuwa serikali haitambui mauaji ya kiholela wala kupotea kwa watu kwa njia zisizoeleweka.
“Serikali inajua tuu kutoa huduma bora kwa wananchi na kuhakikishia wanaishi salama. Wala sio mauaji ya kiholela ama kupotea kwa njia ya kutatanisha,” alisema Kibicho.
Kibicho pia alisema kuwa sharti kambi ya Daadab ifungwe mwishoni mwa mwezi wa kumi na moja.