Mwakilishi wa wadi ya Subukia Peter Muchiri Mwanjo amewashutumu wakuu wa polisi wa kaunti ndogo ya Subukia, kwa kuruhusu vilabu kuendeleza biashara bila kuzingatia sheria ya vileo.
Mwanjo pia amewasuta wakuu hao kwa kudinda kumchukulia hatua za kisheria mpishi mmoja sugu ambaye anaendesha biashara ya upishi na uuzaji wa pombe haramu ya chang’aa.
“Huyo jamaa kutoka eneo la Gatongu amegeuza chumba cha kukuza vyakula (green house) kuwa handaki la upishi wa chang’aa na kuiuza katika eneo hilo pamoja na Miloreni. Inaonekana polisi wanamkingia kifua mpishi huyu kwani licha ya kupewa habari kumhusu na hachukuliwi hatua za kisheria,” alisema Mwanjo.
Akizungumza jana katika kituo cha kibaishara cha Subukia, mwakilishi huyo alidai vijana wanaonekana katika eneo hilo wakiwa walevi masaa ya asubuhi, jambo linalo ashiria kuwa baadhi ya vilabu vinauza pombe mchana kutwa pasipo kuzingatia sheria ya vileo almaarufu kama Mututho law.
“Tunaomba naibu kamishna awachukulie hatua watu wanaouza pombe haramu ili kusaidia vijana wetu wanaojiingiza kwa ulevi,” alisema Mwanjo.
Wakati tulipo wasiliana na mkuu wa polisi Alex Ng’anga, mkuu huyo alisema baadhi ya vilabu vinavyo uza pombe pia ni hoteli na zimepewa kibali cha kuendesha biashara hiyo, lakini huenda baadhi wanafanya kinyume kama inavyo stahili.
Hata hiyo, Ng’ang’a alisema wameanzisha uchunguzi kuhusiana na madai ya mwakilishi huyo.