Kwa muda wa wiki moja sasa, wafanyabiashara wilayani Likoni, Kaunti ya Mombasa, wamekuwa wakiendesha biashara zao kwa hofu baada ya genge moja la majambazi kuanza kuwavamia nyakati za usiku.
Genge hilo linaloaminika kuwa la watu watatu, limekuwa likitembea usiku huku wakiwa wamejihami kwa silaha, na kulenga maduka ya M-Pesa.
Polisi eneo hilo wameanzisha msako dhidi ya genge hilo ambalo limekuwa tishio, sio tu kwa wafanyibiashara bali pia kwa polisi wenyewe.
Usiku wa kuamkia Jumamosi, majambazi hao waliokuwa wamejihami kwa bunduki, walivamia maduka matatu ya M-Pesa huko Likoni na kuiba pesa.
Washukiwa hao waliiba kiasi cha shilingi 40, 000 kutoka kwa duka la M-Pesa eneo la Dudus, Majengo Mapya.
Katika kisa cha pili, washukiwa hao waliingia katika duka la kuuza nyama na kuiba shilingi 9, 000 kabla ya kutoroka.
Akizungumza na waandishi wa habari katika eneo hilo, mkuu wa upelelezi wa Likoni David Siele, alisema vitengo vya usalama vimeanzisha msako mkali na wanamatumani ya kuwanasa washukiwa hao.
Visa hivyo vinajiri wiki kadhaa tu baada ya mwanamke mmoja kuuawa kwa kupigwa risasi kabla ya washukiwa kutoroka na shilingi 90, 000.