Mahakama ya Mombasa imetoa agizo la kukamatwa kwa mshukiwa mmoja wa mauaji, baada ya kususia kuhudhuria vikao vya kesi yake.
Mshukiwa huyo, Joseph Kamau, anadaiwa kumuua mchumba wake Lavin Muya, mnamo Julai 14 mwaka wa 2011, katika eneo la Likoni.
Kamau amekuwa akikosa vikao vya kesi kwa muda sasa, pasi kutoa sababu zozote.
Maafisa wa usalama sasa wamelazimika kuanza msako wa kumtafuta mshukiwa huyo, ili sheria imkabili.
Kutokana na hili, wakili Pascal Nabwana ametishia kujiondoa kwenye kesi hiyo, baada ya mshukiwa huyo kutoroka.
Nabwana ameomba muda wa wiki moja ili kumtafuta mshukiwa huyo, huku akisema kuwa iwapo hatapatikana, basi atajiondoa kwenye kesi hiyo.
Kesi hiyo itatajwa Agosti 18, mwaka huu.