Kamanda wa polisi katika Kaunti ya Nakuru John Koki ametetea kikosi cha polisi dhidi ya lalama za wakaazi ambao wanaendelea kushutumu idara hiyo wakidai haifanyi uchunguzi wa kina pamoja na kufuatilia mienendo ya wahalifu ambao majina yao hutolewa kwa maafisa wa polisi na raia.
Wengi wa wakaazi katika jimbo la Nakuru wamedai baadhi ya habari muhimu ambazo hukabidhiwa idara ya polisi hupuuzwa, jambo ambalo hutilia shime ongezeko la visa vya uhalifu haswa wizi wa magari pamoja na kuvunjwa kwa nyumban na maduka katika mitaa mbali mbali kaunti ya Nakuru.
Hata hivyo mkuu huyo wa polisi ametilia shaka tetesi hizo akisema sheria zinazo heshimu haki na Uhuru wa kimsingi kwa kila mtu zimekuwa kizingiti kikubwa kwa idara ya usalama katika harakati zake za kupiga shoka jinamizi la uhalifu na utovu wa usalama.
Koki amesema sheria inayopendekeza washukiwa kufikishwa mahakamani kabla ya saa 24 ni mojawapo ya shinikizo kandamizi ambazo hulemaza uchunguzi wa polisi dhidi ya wahalifu wanaotiwa nguvuni.
Amesema muda wa saa 24 ni finyu na hauwezi saidia maafisa wa polisi kufanya uchuguzi wa maana pamoja na kutafuta mashahidi haswa katika kesi zenye utata.
Ametaja kesi kama zile za wizi wa mambavu , upatikanaji na silaha hatari, ulanguzi wa dawa za kulevya pamoja na ugaidi kama baadhi ya mashtaka ambayo yanahitaji muda zaidi kuchunguza na kuleta mbele mashahidi ili kuwezesha mahakama kukabiliana na washukiwa kwa mujibu wa sheria.
Kamanda huyo vile vile amesema idara ya mahakama huchangia katika vita dhidi ya uhalifu ingawa sheria huwapa washukiwa nafasi ya kuwa huru kwa dhamana jambo ambalo idara ya polisi na mahakama haziwezi kuepuka.
Amesema baadhi ya washukiwa hutumia nafasi hiyo kuvuruga kesi inayowakabili pamoja na kuwalai mashahidi kususia kesi na kuipa mwanya mahakama kutupilia mbali kesi hiyo.
Koki amesema changamoto sampuli hii hufanya hata wahusika katika kesi kushauriana na kuskizana nje ya mizani ya mahakama akisema wakenya wengi hupendelea mtindo huo wa maskizano kuhujumu haki.
Aidha, koki amewataka wananchi kujihisisha kikamilifu na mpango wa usalama kupitia Nyumba kumi akisema iwapo wananchi watakubatia mpango huo uhalifu utapungua .
Amesema iwapo makundi ya watu jirani watafahamiana itakuwa vigumu wahalifu kuishi miongoni mwao.