Wafuasi wa muungano wa Cord tawi la Nyamira wamefanya maandamano ya amani mjini Nyamira ili kushinikiza makamishna wa tume ya uchaguzi na mipaka kuondoka ofisini. 

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wakiwahutubia wanahabari siku ya Jumatatu mjini Nyamira, wafuasi hao, wakiongozwa na mmoja wa viongozi wa vijana wa chama cha ODM Nyamira Duke Nyagari, wafuasi hao walisema sharti makamishna wa tume hiyo waondoke ofisini.

"Muungano wa Cord na mashirika mbalimbali yasiyo ya serikali yamekosa imani na tume ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC na sharti makamishna hao waondoke afisini kwa haraka ili tuwe na tume huru ya kusimamia uchaguzi," alisema Nyagari. 

Nyagari aidha aliwataka wakenya kote nchini kuungana na muungano wa Cord kwenye azma ya muungano huo kuitaka tume hiyo kuondoka ofisini. 

"Hatuwezi kubali uchaguzi kuendeshwa na tume ambayo tayari wakenya wengi wamekosa imani nao, na kwa sababu hiyo, ni himizo langu kwa wakenya wenzangu kushirikiana nasi kwenye azma ya kuwataka makamishna hao kuondoka ofisini," aliongezea Nyagari. 

Hata hivyo, maandamano hayo yalizimwa na maafisa wa polisi wa kukabiliana na ghasia muda mchache kabla ya waandamanaji hao kufika kwenye ofisi za tume hiyo Nyamira.