Maafisa wa usalama mjini Nakuru usiku wa kuamkia Alhamisi waliwaua majambazi wawili sugu katika eneo la Naivas kwenye barabara kuu ya Nakuru-Nairobi.

Share news tips with us here at Hivisasa

Wawili hao waliuliwa baada ya kukataa amri ya polisi ya kujaribu kuwasimamisha wakiwa ndani ya gari ndogo katika harakati zao za kutokea mjini Nakuru.

Kulingana na kamanda wa polisi jimbo la Nakuru Hassan Barua ni kuwa wawili hao, wanashukiwa kuwa majambazi waliohusika katika wizi kwenye kituo kimoja cha petroli katika eneo la Njoro mapema Jumanne usiku.

"Tulitambua gari lao baada ya kisa hicho cha Njoro na kuulazimu maafisa wa polisi kuwafuata kwa uchunguzi," aliongeza Barua.

Amesema kuwa wawili hao walianza kuwafyatulia polisi pindi walipogundua wanafuatwa kisa kilichowalazimu maafisa wake kuwafyatulia risasi na kuwaua.

"Tumeweza kupata  bunduki aina ya AK47 na bunduki moja bandia, bastola  na vifaa vingine haramu  kutoka kwa gari la washukiwa hawa," alisema Barua.

Miili ya wawili hao imehifadhiwa katika ufuo wa hospitali ya jimbo mjini Nakuru.