Kufuatia kisa cha usiku wa kuamkia siku ya Alhamisi ambapo mwanamke mmoja alimchapa mwanawe wa kike hadi kufariki, sasa maafisa wa polisi wanawashauri wazazi kuwalinda watoto wao vyema na kuwaepusha na visa vya unyanyasaji.
Afisa mkuu wa polisi eneo la Likoni Willy Simba amesema kuwa iwapo wazazi watawalinda vyema watoto wao, basi wataishi vyema nao na watawasaidia katika siku za usoni kwani watakuwa wamepata ulezi bora kutoka kwa wazazi wao.
Akizungumza na wanahabari katika enoe la Likoni siku ya Ijumaa, Simba alisema kuwa jukumu la mzazi ni kuhakikisha kuwa mtoto amepata malezi bora maishani, huku akiwaonya wazazi kujitenga na ugomvi wa kinyumbani na kuishi kwa amani.
Amesema kuwa ugomvi wa mara kwa mara huchangia familia ikakosa amani na kusababisha hasara kubwa kufuatia kuwepo kwa mizozo mingi.
“Tunawaomba wazazi kuwalinda watoto wao vyema na kujiepusha na mizozo ya kifamilia ya mara kwa mara ambayo huchangia kuchipuka kwa hasara kubwa hata mauaji,” alisema Simba.
Kwa sasa afisa huyo mkuu wa polisi anawataka wazazi kushirikiana vyema na kuwalinda watoto wao sambamba na kuwalipia elimu bora ili kuwasaidia katika siku za usoni.
Afisa mkuu wa Polisi eneo la Likoni Willy Simba akizungumza na wanahabari katika eneo la Likoni. Amewashauri wakazi kuwalinda wanao vyema ili wawe watu wa maana siku za baadae. Maktaba