Mamlaka ya kupambana na pombe na dawa za kulevya nchini NACADA, sasa imetoa onyo kwa wanabiashara wanaoingiza nchini kutoka mataifa ya nje pombe isiyo halali.
Mwenyekiti wa NACADA John Mututho, amesema “Pombe hizo haswa hutolewa nchini Uchina, lakini siku za wanabiashara hao bandia zimefikia 40, tutawakamata wote na kuwashtaki mahakamani”.
NACADA imehofia ongezeko la wanabiashara wa kuuza vileo, wanaotaka utajiri wa haraka kwa kukwepa sheria.
“Tayari tumeandikia serikali ya Uchina barua kupitia ubalozi wake hapa nchini kuhusiana na tukio hilo” Mututho akasema.
Akizungumza Alhamisi mjini Naivasha, Mututho alisema NACADA imo kwenye harakati za kununua mashine za kisasa zitakazoweza kukagua vileo ambavyo ni bandia kwa urahisi.
“Ili kupambana na pombe aina hiyo, ni lazima kama NACADA tushirikieni na serikali ya Uchina, na zingine ambapo pombe hii inayodhuru maisha ya wengi hususan vijana inatoka” akasema mbunge huyo wa zamani wa Naivasha.