Tume ya Utumishi wa Umma (PSC) imekanusha madai kwamba Mbunge wa Kabete Ferdinand Waititu alikuwa mfanyakazi wa tume hiyo kwa wakati mmoja.
Katika taarifa kutoka PSC iliyotiwa saini na Alice Otwala, tume hiyo ilisema kuwa hakuna rekodi za kuonyesha kwamba mwanasiasa huyo ana stakabadhi zozote za ajira.
"Tume hii haina rekodi yoyote ya ajira ya Bw Fredinand Ndung'u Waititu ya mnamo Januari 16, 1989," taarifa hiyo ilisema.
Hapo awali, utata ulijitokeza baada ya madai kuibuka kwamba Waititu sio Clifford Ndung'u Waititu ambaye jina lake liko kwenye vyeti hivyo vya shule.
Katika kesi iliyowasilishwa na Gavana wa Kiambu William Kabogo, gavana huyo alisema kuwa "Ferdinand Waititu Ndung'u, ambaye alizaliwa Januari 4, 1980, hawezi kuwa Clifford aliyefanya mtihani wake wa CPE katika Shule ya msingi ya Mbagathi mwaka 1975."
Waititu kwa upande wake alisema kuwa aliamua kubadilisha jina lake kabla ya uchaguzi mkuu wa 2013 kutoka Ferdinand Waititu Ndung'u na kuwa Ferdinand Waititu Clifford Ndung'u.
Kabogo alidai kuwa mbunge huyo alibadili jina lake mwaka 2013 ili kupata vyeti vya shule vinavyoohitajika ili kuwania kiti cha ugavana.
Stakabadhi katika hati ya kiapo ya Kabogo kutoka Chuo Kikuu cha Panjab inasema kwamba jina la Waititu haliko katika rekodi zao.
"Jina la Ferdinand Waititu haliko katika rekodi za wanafunzi waliohitimu Shahada ya Biashara kati ya mwaka 1985-1988. Mwanafunzi mwenye nambari ya usajili ya 85-GC-555 ni Clifford Ndung'u Waititu,” ilisema hati hiyo ya kiapo.
Mbunge wa Kabete Ferdinand Waititu amemtaka Gavana wa Kiambu William Kabogo kujiandaa kwa mashindano magumu mwaka 2017.
Hata hivyo, Waititu ametupilia mbali madai ya Kabogo na kusema kuwa ana wanafunzi wenzake wapatao hamsini kutoka Shule ya Msingi ya Mbagathi na Chuo Kikuu cha Panjab nchini India watakaothibitisha kuwa alienda shuleni.
"Kabogo hapaswi kuogopa ugombea wangu wa mwaka 2017 na badala yake kujiandaa ipasavyo. Nilienda chuo kikuu na hata nikafanya kozi ya tarakilishi,” alisema Waititu.
Sasa wapiga kura wanasubiri kuona matokeo ya mzozo baina ya viongozi hao wawili.