Viongozi mbali mbali katika Kaunti ya Nakuru wameendelea kutofautiana na mapendekezo yaliyotolewa na kiongozi wa waliowengi kwenye bunge la kitaifa Aden Duale ya kutaka serikali kugatua idara ya elimu nchini.

Share news tips with us here at Hivisasa

Wakiongea katika vikao tofauti, mbunge wa Kuresoi kaskazini Moses Cheboi na mwezake wa Molo Jacob Macharia wametofautiana na mapendekezo ya Duale huku wakisema kugatua huduma za elimu itakuwa ni kusambaratisha masomo katika shule za umma.

Hatua ambayo wabunge hao wamedai kwamba itapelekea kushuka kwa viwango vya elimu nchini.

Viongozi hao pia wamesema kuwa baadhi ya huduma ambazo zimegatuliwa ikiwemo ile ya afya zimekuwa changamoto kwa usimamizi wa serikali za kaunti baada ya wahudumu wa afya katika kaunti mbali mbali kufanya migomo ya mara kwa mara wakidai kunyanyaswa na serikali za majimbo.

Macharia ambaye ni mwanakamati ya bunge kuhusu elimu amesema serikali za kaunti hazina uwezo wa kusimamia sekta ya elimu, kwa hivyo mapendekezo ya Duale yanafa kupuuzwa kulingana naye.

Amesema kwa sasa ni serikali kuu pekee ambayo ina uwezo wa kusimamia elimu nchini pamoja na kuhakikisha wanafunzi wanatahiniwa inavyostahili.