Kinara wa Cord Raila Odinga amepuzilia mbali madai ya Naibu Rais William Ruto kuwa Pwani ni ngome ya chama cha Jubilee.
Akizungumza siku ya Jumatano katika Kaunti ya Kilifi, Raila aliitaka Jubilee kutobabaika na kusubiri uamuzi wa wananchi katika uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.
“Jubilee ina wasiwasi kuhusu eneo la Pwani. Heri wasubiri wananchi kuamua wakati wa kura,” alisema Raila.
Ameitaka jubilee kutekeleza maendeleo kwa wananchi badala ya kukashifu vyama vya upinzani.
“Jubilee imeshindwa kufanya maendeleo kwa wananchi na kuanza kugombana na upinzani,” alisema Raila.
Wakati huo huo, kiongozi huyo wa chama cha ODM alisema kuwa bado wakaazi wa Pwani wanakumbwa na dhulma za kihistoria ambazo ndizo vizingiti vya maendeleo.