Mbunge wa Kisauni Ali Mbogo ameelezea kufurahia kwake baada ya mpinzani wake, Rashid Bedzimba kuiondoa mahakamani kesi iliyopinga kuchaguliwa kuchaguliwa wake Agosti 8, mwaka jana.
Bedzimba aliyekuwa bunge hapo awali, alikiwania kiti cha ubunge wa Kisauni kupitia chama cha ODM, lakini akabwagwa naye Mbogo wa Wiper Democratic Movement.
Hapo Jumatatu, mbunge huyo wa zamani ambaye ni rafiki wa karibu wa Gavana Hassan Joho aliiondoa kesi hiyo mahakamani.
Mbogo kisha akauacha ujumbe ufuatao:
"Assalam Aleykum.
Mimi nataka kuchukua fursa hii kumshukuru ndugu yangu mkubwa na kiongozi kwa uamuzi mkubwa wa busara na kishujaa alioufanya hivi leo kwa kuondoa kesi mahakamani.
Sasa jambo la muhimu ni mimi na Hon Rashid Juma Bedzimba kushikana mkono na kuunganisha watu wetu wa Kisauni ili tuweze kutembea barabara moja ya kusameheana, kukuza undugu wetu na kuwafanyia maendeleo watu wetu wa Kisauni.
Mimi nasema asante sana Hon Rashid Juma Bedzimba kwa hii zawadi kubwa uliotupa katika mwezi huu mtukufu.
Nataka nikupe hakikisho langu mimi niko tayari kufanya kazi na wewe ili kujenga Kisauni yetu.
God bless you Big Brother."