Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Kesi ya raia mmoja kutoka nchi jirani ya Tanzania ambaye alinaswa akiwa na dawa za kulevya aina ya Heroin iliendelea siku ya Jumanne katika mahakama makuu yaMombasa, huku upande wa mashtaka ukikataa ombi la raia huyo kupewa dhamana.

Kulingana na mwendesha kesi hiyo Simon Waithaka alidai kuwa iwapo mshtakiwa atapewa dhamana huenda akatoroka ikizingatiwa kuwa anatoka katika nchi jirani na itakuwa vigumu kufuatiliwa.

“Itakuwa vigumu kupatikana iwapo atatoweka ikizingatiwa kuwa hii ni kesi nzito ya mihadarati za zaidi ya shilingi milioni nane,” alisema Waithaka.

Mshukiwa huyo alishikwa na maafisa wa idara ya ushuru katika mpaka wa Kenya na Tanzania kwa ushirikiano na maafisa kutoka kituo cha polisi cha Lunga Lunga mnamo tarehe 18 mwezi wa pili mwaka huu akiwa na zaidi ya gramu 2,000 zenye thamani ya shilingi za Kenya takribani milioni nane.

Kesi hiyo ambayo ilianza kusikilizwa siku ya Jumatatu ambapo upande wa mashtaka kulingana na mwendesha kesi hiyo unatarajiwa kuwasilisha mashahidi sita ili kutoa ushuhuda kwenye kesi hiyo, na kufika siku ya Jumanne shahidi wa pili ndiye alikuwa akitoa ushahidi wake kama afisa ambaye alimtia mbaroni mshukiwa.

Hakimu alisimamia kesi hiyo Richard Ondenyo aliahirisha kesi hiyo hadi mwaka ujao tarehe kumi na tano mwezi wa kwanza.