Kinara wa Mrengo wa upinzani nchini CORD, Raila Odinga amewashauri vijana watumie ujuzi walio nao ili waweze kujikimu kimaisha kupitia ubunifu wa ajira.
Akiwahutubia vijana kwenye kongamano la vijana mjini Mombasa siku ya Jumamosi, Raila alisema kuwa vijana wanafaa kuwa mstari wa mbele kupigania demokrasia na kulinda katiba ya nchi.
Raila aliilaumu serikali ya Jubilee akidai kuwa inatoa ajira kwa misingi ya kikabila, huku mamia ya vijana wakikosa nafasi hizo za kazi.
"Serikali ya Jubilee inawanyanyasa wakenya na kuwakandamiza kwa kuwanyima ajira na kuajiri watu wa kabila fulani, hiyo sisi hatutakubali kabisa,” alisema Raila.
Aidha alitoa mwito kwa wakenya waige mfano wa nchi jirani ya Tanzania, akisema kuwa Rais wa nchi hiyo John Pombe Magufuli alichaguliwa kutoka kwa kabila la watu walio wachache katika nchi hiyo.
Kongamano hilo lilihudhuriwa na Gavana wa Kaunti ya Mombasa Ali Hassan Joho, miongoni mwa viongozi wengine wakuu wa mrengo wa Cord.