Kinara wa muungano wa upinzani Raila Odinga amekanusha madai yaliyoenea kwa vyombo vya habari kuwa atawania kiti cha urais kutumia tiketi ya moja kwa moja ya mrengo wa Cord.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Raila amesema kuwa huo ni uvumi unaonuia kuzua mgogoro baina ya viongozi tanzu wa chama hicho.

Kwenye taarifa katika vyombo vya habari, Raila alisema kuwa atafuata uamuzi wa chama hicho na kwamba hatma yake ya kuwania kiti cha urais itategemea namna mrengo huo utakavyofanya uteuzi wake, kulingana na sheria na utaratibu uliowekwa na vyama tanzu vinavyojumuisha mrengo huo.

Baadhi ya taarifa kwenye vyombo vya habari zilidai kuwa Raila kama kiongozi mkuu wa chama cha ODM, anapania kupeperusha bendera ya mrengo huo licha ya kwamba waliafikiana kuwa kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka atachukua nafasi hiyo na kugombea kiti cha urais mwaka ujao.

Seneta wa Bungoma James Orengo na mwakilishi wa wanawake Kaunti ya Mombasa Mishi Mboko wamesema kuwa uvumi huo unanuia kuharibia mrengo huo sifa.

Hata hivyo, Orengo amesema itakuwa vyema kwa Kalonzo kutwaa nafasi hiyo na kupeperusha bendera ya muungano huo kwani ashawahi kuhudumu katika serikali kama naibu rais.

Mboko kwa upande wake alisema kuwa muungano wa Cord utaandaa kikao cha kuwachagua wajumbe watakaoingia kwenye debe la mwaka ujao.