Kiongozi wa muungano wa upinzani CORD Raila Odinga ameitaka jamii ya Waluhya kustahimili majaribio ya pesa kutoka serikali ya Jubilee.
Akiwahutubia wafuasi wa ODM waliojitokeza kumskiza eneo la Chavakali kaunti ya Vihiga, Raila amekanusha madai kwamba hajaisaidia jamii hiyo, huku akihesabu yale ambayo aliifanyia jamii hiyo akiwa waziri mkuu.
Raila aliongeza kuwa akiwa waziri mkuu, jamii hiyo ilikuwa na wawakilishi wengi serikalini kuliko ilivyo sasa katika serikali ya Jubilee.
Raila alijaribu kukwepa suala la Ababu Namwamba lakini aliposukumwa kulizungumzia, alimwambia mbunge huyo wa Budalangi arejee nyumbani .
Awali akiongea Vihiga baada ya kuanza ziara ya siku tanu katika eneo la magharibi, Raila alidai utawala wa Jubilee umeweka taifa hili katika madeni kubwa.
Vile vile Raila amemshutumu naibu wa Rais William Ruto kwa madai ya kutumia pesa za uma katika michango ya harambee anayozunguka akifanya kote nchini ilihali hakuna maendeleo yoyote yanayoonekana.
Ziara ya kiongozi wa upinzani Raila Odinga inawadia siku chache baada ya msukosuko kukikumba chama cha ODM ambacho ni mojawapo ya vyama katiaka muungano wa CORD.
Ziara hiyo pia imechochewa na wabunge Ababu Namwamba (Budalangi) na John Waluke (Sirisia) kujiuzulu nyadhifa zao katika chama cha ODM na kukisia kukihama chama hicho.